
Episode #23
Mungu Hakuiti Bila Kukupa Uwezo!
️ Leo kwenye Neno la Leo Leo kupitia 1 Samweli 10:6 tunamwona Sauli akikabiliwa na jambo kubwa kuliko maisha aliyokuwa ameyazoea. Mungu alikuwa anamwita kwenye jukumu jipya lakini hakutarajia Sauli alibebe kwa nguvu zake mwenyewe. Samweli anamwambia, “Roho wa Bwana atakujilia kwa nguvu” na kwamba Sauli atabadilishwa kuwa mtu mwingine. Mungu aliyemwita alikuwa pia anaenda kumwandaa na kumwezesha. Neno la leo linatukumbusha kwamba wakati mwingine Mungu anaweza kutupeleka kwenye majukumu yanayotufanya tujiulize, “Mimi nitawezaje?” Tunaweza kuangalia uwezo wetu, uzoefu wetu au mapungufu yetu na kujiona hatutoshi. Lakini wito wa Mungu hautegemei uwezo wetu pekee. Mungu anapokuita, anakupa pia neema na nguvu unazohitaji kutekeleza kile alichoweka mbele yako. Hii haimaanishi kwamba hatuhitaji kujifunza, kujiandaa au kufanya kazi kwa bidii. Sauli bado alikuwa na wajibu wa kutii. Lakini hakutakiwa kutegemea nguvu zake peke yake. Hata sisi tunahitaji kuelewa tofauti kati ya kujiamini wenyewe na kumtegemea Mungu anayetuwezesha. Je, kuna jukumu ambalo Mungu ameweka mbele yako lakini unaogopa kwa sababu unajiona huna uwezo wa kutosha? Usiangalie tu ukubwa wa jukumu. Mtazame Mungu aliyekuita. Mungu hakuiti bila kukuwezesha. Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. ✨






